Rais wa zamani wa Marekani, George W. Bush, amekosoa hatua ya kuondolewa kwa vikosi vya majeshi ya Muungano wa Umoja wa Nchi za kujihami (NATO) nchini Afghanistan akisema hatua hiyo inaweka hatarini usalama wa raia kutokana na mauaji ambayo yamekuwa yakifanywa na wanamgambo wa Taliban.
Rais huyo wa zamani wa Marekani ambaye alishiriki kikamilifu katika kuuangusha utawala wa Taliban nchini Afghanistan amesema uamuzi huo ni jambo linalomvunja moyo kwa sababu raia hususan wanawake nchini humo ni kundi ambalo limekuwa likitaabishwa sana na Taliban.
Akiwa Rais kupitia chama cha Republican, Bwana alituma vikosi vya jeshi la Marekani nchini Afghanistan mwaka 2001 kufuatia mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 jijini New York aliyosisitiza kuwa yalitekelezwa na kundi la Taliban likiongozwa na Osama Bin Laden.
Aidha amesema anaamini Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ana mtazamo kama wake kuhusiana na suala hilo ambapo pia amempongeza Kansela huyo kwa maamuzi yake ya kupeleka majeshi ya Ujerumani nchini Afghanistan wakati huo.