Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa licha ya mvua zinazoendelea kunyesha nchini, Bwala la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) lipo salama kutokana na kujengwa kisayansi na hivyo kuendelea kuzalisha umeme kupitia mtambo namba tisa huku mitambo mingine miwili ikiwa ukingoni kukamilika.
Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 18 Aprili 2024 jijini Dodoma katika mahojiano Mbashara kupitia kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC kuhusu Maonesho ya Wiki ya Nishati 2024 yanayoendelea katika Viwanja vya Bunge.
“ Bwawa letu lipo salama kwani limejengwa kisayansi, ujazo wake wa maji ni mita za ujazo 183 na kwa takwimu za leo ni mita za ujazo 183.4, huko nyuma maji yalikuwa yakiingia mengi sana kwa kiasi cha mita za ujazo 8400 kwa sekunde hivyo yalipaswa kupunguzwa ili kuendana na ujazo wa bwawa.” Amesema Dkt. Biteko
Amesema kuwa, bila ya kuwepo kwa Bwawa hilo athari za mvua zingeanza kuonekana tangu mwezi Oktoba mwaka jana lakini hali hiyo haikutokea mapema kwa sababu maji yalikuwa yakiijazwa katika bwawa kwa ajili ya kuzalisha umeme.
Ameongeza kuwa, Wizara ya Nishati na TANESCO ilishabaini uongezekaji wa maji katika mto Rufiji kuanzia mwezi Februari, mwaka huu na tahadhari ilianza kutolewa kuhusu kasi hiyo ya maji ili kuanza kuchukua hatua stahiki.