Bweni la wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Waadventista wa Sabato Tanzania iliyopo Usa river wilayani Arumeru Mkoani Arusha limeteketea kwa moto na kuunguza vifaa mbalimbali vya wanafunzi.
Moto huo umetokea jana mchana wakati wanafunzi wa shule hiyo wakiwa madarasani na uchunguzi wa kupata chanzo cha moto huo bado unaendelea.
Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilayani Arumeru Mkaguzi Alhaji Kimaro ameeleza vifaa mbalimbali vya wanafunzi katika vyumba 14 vimeteketea kabisa na moto kati ya vyumba 30 vilivyopo katika bweni hilo.
Kwa upande wake mmoja wa shuhuda wa tukio hilo David Mnyanda ameeleza hali ilivyokuwa baada ya kubaini kwamba kuna tukio la moto katika bweni hilo.
Mkuu wa shule hiyo Mborega Petro amewaomba wasamaria wema kuwasaidia kwa hali na mali wanafunzi ambao wamepoteza vifaa vyao vya matumizi ya kila siku ya shuleni hapo.