MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo October 2, 2017 imemuhukumu kifungo cha miaka mitatu jela ama kulipa faini ya Tsh. Milioni 20 Mkurugenzi wa Utafiti na Mipango wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Samweli Mvingira na mwenzake baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kutumia madaraka vibaya.
Mbali ya Mvingira, mwingine aliyehukumiwa na kufanikiwa kulipa faini ni Naibu Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Judith Msuya.
Katika hukumu yake, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha amesema washtakiwa hao wametiwa hatiani baada ya Jamuhuri kuthibitisha mashtaka dhidi yao ambapo alisema amewatia hatiani kwa makosa manne ya kutumia madaraka yao vibaya, lakini pia hawakupatina na hatia katika kosa la tano.
Hakimu Mkeha amesema washtakiwa wanatakiwa kulipa faini ya Tsh. Milioni 5 kuanzia kosa la kwanza hadi la nne na endapo watashindwa wataenda jela miaka mitatu kwa kila kosa.
Katika kesi hiyo washtakiwa walikuwa watatu akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade ambaye alifariki wakati shahidi wa kwanza akitoa ushahidi.
Inadaiwa, kati ya September 2007 na July 2008, Makao Makuu ya TanTrade Wilaya ya Temeke walitumia madaraka yao vibaya kwa kuagiza gari lililotumika kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma iliyosababisha AL Hamadi Motors FZD kupata faida ya Tsh. 34,895,400.
Aidha, inadaiwa tarehe hiyo hiyo na mahali hapo, washtakiwa kwa kutumia madaraka yao vibaya, walinunua gari iliyotumika kwa lengo la kumnufaisha Humer Stars kiasi cha Tsh. 32,773,475.
Washtakiwa wanadaiwa bila kufuata utaratibu wa kushindanisha zabuni kuagiza gari iliyotumika na kusababisha AL Hamad kupata faida ya Tsh. 34,895,400, hata hivyo katika shtaka la nne watuhumiwa walinunua magari bila kufuata utaratibu wa zabuni.
Pia washtakiwa waliachiwa huru ambapo Jamuhuri ilishindwa kuthibitisha, washtakiwa walidaiwa kutumia madaraka yao vibaya, uzembe na kumsababishia mwajiri wao hasara ya Tsh. 49,145,855.05.
BREAKING: Kauli ya Nassari, Lema na Msigwa baada ya kufikisha ushahidi TAKUKURU