Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere, ameongea na Waandishi wa Habari kuhusu ripoti ya ukaguzi wa hesabu 2021/2022 Dodoma leo ambapo amesema Ofisi yake imebaini wanufaika wa mikopo katika Mamlaka 180 za Serikali za Mitaa wameshindwa kurejesha mikopo ya Tsh. Bilioni 88.42.
“Kanuni ya 24 ya Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu za mwaka 2019 inafafanua hatua za kinidhamu kwa atakayetumia mkopo kinyume na shughuli zilizoidhinishwa na Kamati ya Fedha na Mipango au kutoa taarifa za uongo kwa lengo la kujipatia mkopo kuwa atawajibika kulipa faini ya kati ya Tsh. 200,000 na Tsh. 1,000,000 au kifungo kati ya miezi 12 na 24″
“Tathmini yangu juu ya uendeshaji wa Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu nilibaini kuwa, wanufaika wa mikopo katika Mamlaka 180 za Serikali za Mitaa wameshindwa kurejesha mikopo ya Tsh. Bilioni 88.42”
“Kutorejeshwa kwa mikopo husika pamoja na mambo mengine, kumechangiwa na Wahusika kutochukuliwa hatua kali za kisheria zitakazowasukuma walazimike kurejesha mikopo hiyo, ninapendekeza TAMISEMI iongeze udhibiti ndani ya mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wanavikundi wanaokiuka mikataba ya mikopo”