Mchezaji wa kikosi cha Cameroon katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ni miongoni mwa wachezaji 52 wanaokabiliwa na kutengwa katika mchujo wa kuwania kufuzu kwa michuano ya ligi kuu ya nchi hiyo kutokana na kasoro za usajili wao.
Wilfried Nathan Douala na wachezaji wengine 51 wanaochukuliwa na Shirikisho la Soka la Cameroon kuwa na “utambulisho maradufu” walidanganya kuhusu umri wao na walisimamishwa, idhaa ya Ufaransa ya RMC na vyombo vya habari vya Cameroon viliripoti Jumatatu.
Klabu moja pekee – Yong Sports Academy – imekuwa na wachezaji 13 walioangaziwa kwa kusimamishwa au utambulisho wa watu wawili.
Shirikisho hilo lilichapisha siku ya Jumapili orodha za timu zitakazoshiriki mchujo huo unaotarajiwa kuanza Ijumaa, huku majina ya wachezaji 52 yakiangaziwa kwa rangi nyekundu kwa “utambulisho maradufu”.
Douala anayechezea klabu ya Victoria United FC ana umri wa miaka 17 kwa mujibu wa usajili wake.