Wachezaji muhimu wa Real Madrid , Cristiano Ronaldo na Iker Casillas wameripotiwa kuwa mbioni kuihama klabu hiyo mara baada ya kumalizika kwa msimu huu .
Wachezaji hao wawili kila mmoja kwa wakati wake tofauti wameripotiwa kuwa na mpango wa kuihama klabu hiyo kwa sababu tofauti huku kukiwa hakuna taarifa yoyote rasmi inayowahusisha na timu ambazo wanaweza kujiunga nazo .
Kauli ya kipa wa zamani wa Real Madrid Agustin rodriguez ambaye alinukuliwa na jarida la Marca akisema kuwa ana uhakika kuwa wachezaji hao wawili watahama imezua utata mkubwa kwenye magazeti kadhaa barani ulaya .
Casillas ambaye kwa karibu misimu mitatu amekuwa akicheza chini ya kiwango amekuwa na wasiwasi mkubwa juu ya nafasi yake kama kipa namba moja wa Real Madrid baada ya kuwepo kwa tetesi kadhaa zinazoihusisha Real na mpango wa kumsajili kipa wa Manchester United David De Gea .
Vyombo vya habari tofauti vimekuwa vikiwahusisha Madrid na mpango wa kumsajili De Gea ambaye ametajwa kuwa tayari kurudi nyumbani kwao jijini Madrid ambako Real imemuahidi nafasi katika kikosi chake cha kwanza .
Hata hali ni tofauti kwa Ronaldo ambaye tetesi za kuhama kwake hazijasikika sana kwa msimu huu kama ilivyokuwa msimu uliopita wakati akiwa hajasaini mkataba wake mpya ambapo alihusishwa na kurejea kwenye klabu ya Manchester United .