Mkuu wa utawala wa jeshi nchini Chad, Jenerali Mahamat Idriss Déby Itno Jumatatu aliwasamehe waandamanaji 259 kati ya 262 waliohukumiwa kifungo gerezani baada ya maandamano dhidi ya utawala yaliyokandamizwa kwa umwagaji damu mnamo mwezi Oktoba 2022, siku tatu baada ya agizo kama hilo lililowaachia huru waasi 380 waliohukumiwa kifungo cha maisha.
Waandamanaji hawa walihukumiwa katika kesi ya halaiki iliyofunguliwa mwezi Desemba, bila wanasheria au vyombo vya habari huru, na baada ya zaidi ya mwezi mmoja na nusu kuzuiliwa katika gereza lenye ulinzi mkali katikati mwa jangwa nchini Chad kilomita 600 kutoka mji mkuu N’Djamena
Wafungwa hawa, wengi wao wakiwa vijana, walikuwa wameitikia mwito wa kupinga kuongezwa kwa miaka miwili madarakani kwa Jenerali Déby mwezi Oktoba.
Uchunguzi bado unaendelea kwa watu “ishirini” waliozuiliwa N’Djamena, na wengine “mia moja ” katika gereza la Koro Toro, alisema Laguerre Ndjerandi, kiongozi wa chama cha majaji huko N’Djamena.
“Ni ishara ya msamaha kuwaruhusu wana na mabinti wote wa Chad kujenga nchi yao katika misingi mipya,” waziri wa mawasiliano na msemaji wa serikali Aziz Mahamat Saleh ameliambia shirika la habari la AFP.