Tanzania na Zambia zimekubali kutatua changamoto 25 za kibiashara zilizopo ifikapo Novemba 30, 2023 ili kuiwezesha sekta binafsi kufanya biashara bila vikwazo vyovyote baina ya nchi hizo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dkt. Ashatu Kijaji na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Zambia Mhe. Chipoka Mulenga wa Zambia wakiwa pamoja na Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Mwakiposya Kihenzile (Mb.) walipokutana na kushiriki Mkutano wa Pili wa Pamoja wa Kujadili Changamoto za Biashara baina ya nchi hizo ngazi ya Mawaziri uliofanyika katika Mpaka wa Nakonde, Zambia Novemba 07, 2023.
Aidha, Dkt. Kijaji amesema makubaliano ya kutatua changamoto hizo yanatokana na utekelezaji wa Maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokutana na Rais wa Zambia Mhe. Hakainde Hichilema katika ziara ya Kitaifa nchini humo Oktoba 23 – 25, 2023 na kukubaliana kuiwezesha Sekta Binafsi kufanya biashara baina ya nchi hizo.
Aidha, amesema nchi hizo pia zimekubaliana kutatua changamoto hizo kwa haraka na kuhakikisha kuwa kila changamoto inayojitokeza baina ya nchi hizo itatatuliwa ili kuiwezesha sekta binafsi kufanya biashara kwa uhuru ili kukuza biashara na uchumi wa nchi hizo kwa kuwa Sekta Binafsi ni injini ya kukuza uchumi kwa mataifa yote mawili
Naye Waziri Mulenga amesema nchi hizo zimekubaliana kutatua changamoto hizo ili kuiwezesha sekta binafsi kujenga uchumi imara chini ya misingi iliyowekwa na Waasisi wa nchi hizo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Kenneth Kaunda iliyoziwezesha nchi hizo kuishi kwa amani na utulivu.