Umoja wa Mataifa umetangaza nyongeza ya chanjo ya malaria barani Afrika baada ya shehena ya kwanza ya dozi kuwasili Cameroon.
Tangu mwaka wa 2019, zaidi ya watoto milioni mbili wamepewa chanjo hiyo nchini Ghana, Kenya na Malawi katika awamu ya majaribio, na kuwa na matokeo mazuri katika kupunguza maambukizi makali ya ugonjwa wa malaria na idadi ya wagonjwa waliolazwa.
Kwa sasa mpango huo umeingia katika usambazaji mkubwa zaidi wa dozi iliyopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ambayo itafika mjini Yaoundé wiki ijayo.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa na Shirika la afya duniani (WHO), Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF, na Muungano wa chanjo (GAVI) imesema utoaji huo “unaashiria ongezeko la chanjo dhidi ya malaria katika maeneo hatarishi zaidi katika bara la Afrika”.