Zaidi ya chanjo milioni moja za polio zilizokusudiwa kutolewa kwa watoto zimeharibiwa ikiwa ni matokeo ya uporaji nchini Sudan.
Hayo ni kwa mujibu Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF).
Uharibifu huo umetokea huku mzozo ukiendelea kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha usaidizi wa haraka uliozuka mwezi Aprili.
Naibu mkurugenzi wa Ofisi ya Mipango ya Dharura katika UNICEF, Hazel De Wet alisema vifaa kadhaa baridi vya kuhifadhi chanjo vimeporwa, kuharibiwa na kuangamizwa huko Darfur Kusini.
Shirika hilo lilikuwa katikati ya kampeni mfululizo za utoaji chanjo ya polio nchini Sudan. Kampeni ambazo zilifuatia mlipuko wa ugonjwa huo mwishoni mwa mwaka 2022.
UNICEF ni miongoni mwa mashirika kadhaa ya misaada ya kibinadamu yaliyoripoti uporaji wakati wa mzozo wa Sudan.
Wakati mapigano ya ndani yakiendelea nchini Sudan, Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa watu milioni 19 nchini humo wanaweza kukumbwa na uhaba wa chakula katika miezi ijayo.
Mapigano makali yalizuka Aprili 15 kati ya kiongozi mkuu wa Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye anaongoza jeshi la kawaida, na naibu wake aliyegeuka mpinzani Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, ambaye anaongoza Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) licha ya kuahidi kusitisha mapigano.