Shirika la afya duniani, WHO limearifu kuwa liko mbioni kufanya majaribio ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Ebola, ambao umeripotiwa kuua takribani watu 4,500 huku nchi za Afrika Magharibi zikiripotiwa kuathirika zaidi tangu kulipuka kwa ugonjwa huo.
Taarifa iliyoripotiwa na CNN imesema kuwa shirika hilo limepanga kuanza utekelezaji wa jaribio hilo mapema Januari mwaka 2015 katika nchi za Afrika Magharibi, huku wakisisitiza kuwa chanjo zote hazina madhara kwa afya ya binadamu, japo chanjo hiyo haitowahusu wagonjwa ambao tayari wana maambukizi Ebola.
Mratibu wa zoezi hilo Dk. Marie Paule Kieny amesema, chanjo hiyo itatolewa kwa mtu yoyote atakayekuwa tayari kujitolea kushiriki.
Amezitaja nchi za Mali, Uingereza na Marekani kuwa ni baadhi ya nchi ambazo jaribio la chanjo hiyo litafanyika.
Shirika la afya limesema limeagiza wataalamu kufanya ziara Afrika Magharibi katika nchi ambazo wananchi wake wameathirika zaidi na ugonjwa huo, ambapo pia ziara hiyo itahusisha pia zoezi la ukaguzi wa vituo ambavyo vitatumika kutolea huduma hiyo ya chanjo.
Iwapo chanjo hii itafanikiwa itafufua matumaini kwa watu wa Afrika ya Magharibi ambao wameshuhudia athari kubwa zilizosababishwa na Ebola ambapo watu zaidi ya 4,500 wameripotiwa kufariki na wengine zaidi ya 9,000 wana maambukizi ya ugonjwa huo.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook