Mshambuliaji wa Chelsea Diego Costa atalazimika kukaa nje ya uwanja akikosa michezo mitatu ya timu hiyo kwenye ligi ya England baada ya kukutwa na hatia ya utovu wa nidhamu kufuatia vitendo kadhaa vya mchezo usio wa kiungwana vilivyoonekana kwenye mchezo dhidi ya Liverpool.
Mshambuliaji huyu wa kimataifa wa Hispania alikutwa na hatia ya kumkanyaga kiungo wa Liverpool Emre Can katika mchezo wa hatua ya nusu fainali ya Capitol 1 Cup ambao Che;sea ilishinda 1-0 na kufuzu hatua ya fainali .
Kamati ya nidhamu ya FA ambayo iliketi siku ya jumatano ilifikia uamuzi huo wa kumfungia Costa kutocheza michezo mitatu huku akipewa fursa ya kukata rufaa rufaa ambayo hata hivyo imetupiliwa mbali
Mshambuliaji huyo alijitetea kuwa hakufanya kitendo hicho kwa kusudi kwani hakuwa ametazama mguu wake umekanyaga sehemu gani na hakuna na lengo la makusudi la kumchezea rafu mchezaji wa Liverpool.
Kwa matokeo haya Chelsea itamkosa Costa kwenye michezo muhimu ya ligi kuu ya England dhidi ya Manchester City , Everton na Aston Villa hali ambayo itakuwa pengo kubwa kwa kocha Jose Mourinho .
Costa hadi sasa amefunga mabao 17 kwenye ligi ya England akiwa anaongoza msimamo wa wafungaji huku akiisadia timu yake kukaa kileleni mwa ligi hiyo huku wakiwazidi wapinzani wao Manchester City kwa pointi 5 .
Pengo kubwa kwa Chelsea wikiendi hii litakuwa kumkosa kiungo mshambuliaji Cesc Fabregas ambaye ana jeraha la misuli ya nyuma ya mguu na Chelsea itakuwa kwenye wakati mgumu sasa kucheza na City bila wahispania hawa wawili Cesc na Diego ambao kwa pamoja wanaongoza kwa mabao na pasi za mwisho .