Serikali ya China imesema leo Jumatatu kuwa “inakanusha vikali” shutuma za ujasusi nchini Uingereza, baada ya kukamatwa huko Edinburgh kwa mtu anayeshukiwa kukusanya taarifa za kijasusi kwa niaba ya Beijing.
“Habari zinzodai kuwa China inaipeleleza Uingereza hayana msingi wowote na China inayafutilia mbali kabisa,” msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Mao Ning amesema katika mkutano wa kila siku na waandishi wa habari.
“Tunahimiza upande wa Uingereza kuacha kueneza habari za uwongo na kukomesha ujanja wao wa kisiasa dhidi ya China na kutupaka matope kwa nia mbaya,” ameongeza.
Siku ya Jumamosi polisi nchini Uingereza ilitangaza kuwa inamshikilia mwanamume mwenye umri wa miaka ishirini aliyekamtwa nyumbani kwake huko Edinburgh kwa ujasusi.
Kulingana na Gazeti la Sunday Times, mtu huyo ni mtafiti ambaye alikuwa na mawasiliano na wabunge wa chama tawala cha Conservative wakati akifanya kazi Bungeni. Msemaji wa ubalozi wa China mjini London, alipoulizwa kuhusu madai hayo, aliyataja kuwa ni “ujajna wa kisiasa.”
chanzo:RFI