Shirika la Afya Duniani siku ya Jumatano liliwataka wakazi wa China kujilinda baada ya kuona ongezeko la magonjwa ya kupumua na milipuko ya nimonia iliyoripotiwa miongoni mwa watoto.
Shirika la Afya Dunianii limeelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa magonjwa ya kupumua nchini China na kuwataka watu “kuchukua hatua za kinga”.
“WHO imetuma ombi rasmi kwa China kwa taarifa za kina juu ya ongezeko la magonjwa ya kupumua na milipuko ya nimonia iliyoripotiwa kwa watoto,” imesema taarifa hiyo iliyochapishwa kwenye mtandao wa X (zamani ikiitwa Twitter) ambayo ukweli wake umethibitishwa kwa shirika la habari la AFP na msemaji wa shirika hilo, ambaye anapendekeza kufuata “hatua zinazolenga kupunguza hatari ya ugonjwa wa kupumua.”
Hatua hizi -ambazo tayari zimeshatolewa wakati wa janga la UVIKO-19 – ni pamoja na chanjo, kujitenga na wagonjwa, kukaa nyumbani ikiwa kuna dalili, vipimo na utunzaji ikiwa ni lazima na kuvaa barakoa ikiwa inafaa, majengo mazuri ya uingizaji hewa na kunawa mikono.