Kocha wa Paris Saint-Germain Christophe Galtier na mwanawe wamezuiliwa kama sehemu ya uchunguzi wa tuhuma za ubaguzi wa rangi katika moja ya klabu zake za zamani, mwendesha mashtaka wa Nice Xavier Bonhomme aliambia The Associated Press.
Galtier na mwanawe, John Valovic-Galtier, waliwekwa chini ya ulinzi kwa mahojiano Ijumaa asubuhi, Bonhomme alisema.
Galtier, ambaye yuko njiani kuondoka PSG lakini bado ana kandarasi, alikanusha shutuma kwamba alitoa maoni ya kibaguzi na chuki dhidi ya Waislamu alipokuwa akisimamia klabu ya Nice ya Ufaransa wakati kashfa hiyo ilipozuka mapema mwaka huu.
RMC Sport na vyombo vingine vya habari vya Ufaransa vilichapisha ripoti zinazonukuu barua pepe iliyovuja kutoka kwa mkurugenzi wa zamani wa soka wa Nice Julien Fournier kwenda kwa wamiliki wa klabu hiyo, ambapo alimshutumu Galtier kwa kusema kuna wachezaji wengi Weusi na Waislamu kwenye kikosi.
Katika taarifa iliyotolewa na wakili wake kwa vyombo vya habari vya Ufaransa, Galtier alisema “alishangaa kusikia ripoti hiyo ya matusi na kashfa” na akasema atachukua hatua za kisheria ambazo hazikutajwa.