Utekelezaji wa Mradi wa HEET unafanyika sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2020-2025).
Kwa pamoja vinalenga katika kuimarisha uchumi wa viwanda ili kuendana na uchumi wa kati, na kuongeza fursa za ajira kwa makundi mbalimbali hususan vijana.
Sisi tunajiona kuwa na bahati kubwa sana kufikiwa na mradi huu kwani unarandana na Dira yetu ya UDSM Vision 2061 na mpango mkakati wa Chuo 2020/21-2024/25.
Dira ya Chuo na Mpango Mkakati vinalenga kufanya mageuzi ya kitaasisi yanayoendana na vipaumbele na mahitaji ya taifa ya sasa na baadaye. Hivyo Utekelezaji wa Mradi wa HEET umejikita kwenye kuimarisha na kuboresha miundombinu, ikiwemo ukarabati mkubwa na ujenzi wa majengo mapya pamoja na kufunga vifaa vipya kwenye majengo haya.
Ni katika muktadha huo, Chuo kinajipanua na kuwafikia Watanzania zaidi kwa kuanzisha Kampasi mpya katika mikoa ya Lindi na Kagera katika fani za Kilimo na Biashara. Aidha ili kuendana na matumizi ya TEHAMA, Chuo kimejipanga kuimarisha miundombinu ya TEHAMA ili kuoboresha ufundishaji na utoaji wa huduma mbalimbali zikiwemo ulinzi na usalama. Matumizi ya TEHAMA yatapewa msisitizo mkubwa kwenye kufundisha na kujifunza.
Timu yetu ya wataalamu imefanya kazi kubwa ya kuandaa michoro, kuiwasilisha kwa wadau na watumiaji wa majengo, kuifanyia marekebisho na kisha kupitishwa na Baraza. Ni matumaini yetu kuwa majengo haya yatakidhi mahitaji yote muhimu ya wakati huu katika miundombinu ya kufundishia na kujifunzia. Wajenzi na wasimamizi wa ujenzi wahakikishe kuwa tunapata majengo bora na ya kisasa.