Chuo Kikuu cha Howard kilifutilia mbali shahada ya heshima ilichomtunuku mwanamuziki maarufu wa hip-hop Sean “Diddy” Combs na kukata uhusiano naye wiki kadhaa baada ya video iliyotolewa hivi majuzi 2016 ikimuonyesha akimshambulia mwimbaji wa R&B na mpenzi wa zamani, Cassie.
Bodi ya Wadhamini ya chuo kikuu hicho ilisema pia ilielekeza wasimamizi kukata uhusiano wa kifedha na Combs, pamoja na kurudisha mchango wa dola milioni 1, kumaliza mpango wa udhamini na kuvunja makubaliano ya ahadi ya 2023 na Wakfu wa Sean Combs.
“Tabia ya Bw. Combs kama ilivyonaswa katika video iliyotolewa hivi majuzi haiendani kimsingi na maadili na imani kuu za Chuo Kikuu cha Howard hivi kwamba anachukuliwa kuwa hastahili tena kushikilia heshima ya juu zaidi ya taasisi,” taarifa ilisema.
Taarifa hiyo ilisema bodi ilipiga kura kwa kauli moja Ijumaa kukubali kurejeshwa kwa digrii ya heshima ya Combs iliyopokelewa mnamo 2014.
“Kukubalika huku kunabatilisha heshima na marupurupu yote yanayohusiana na shahada hiyo. Kwa hivyo, Bodi imeagiza kwamba jina lake liondolewe kwenye hati zote zinazoorodhesha wapokeaji wa shahada ya heshima wa Chuo Kikuu cha Howard,” ilisema.