Polisi wa Kongo walirusha mabomu ya machozi siku ya Jumatano kutawanya maandamano ya wafuasi wa upinzani katika mji mkuu Kinshasa wanaotaka kurudiwa kwa uchaguzi wa rais na wabunge uliokumbwa na machafuko wiki iliyopita.
Kura hiyo inayozozaniwa inatishia kuiyumbisha zaidi Kongo, ambayo tayari inakabiliana na mzozo wa usalama katika eneo la mashariki ambao umetatiza maendeleo katika mzalishaji mkuu wa cobalt duniani na madini mengine ya kiviwanda na metali.
Wapinzani watano wa Rais Felix Tshisekedi katika kinyang’anyiro hicho pamoja na mashirika ya kiraia, walitoa wito kwa wafuasi wao kujiunga na maandamano siku ya Jumatano kupinga uchaguzi huo, ambao wanasema ulikuwa wa udanganyifu na unapaswa kufutwa.
Maandamano ya kupinga mchakato wa uchaguzi yalikuwa yamepigwa marufuku na mamlaka, AFP iliripoti hapo awali.
Waziri wa Mambo ya Ndani Peter Kazadi alitangaza Jumanne kwamba maandamano hayataruhusiwa. “Inalenga kudhoofisha mchakato wa uchaguzi, serikali ya Jamhuri haiwezi kukubali hili,” alitangaza.
Upinzani ulidumisha kauli mbiu yake na kuwataka watu wa Kinshasa kukusanyika karibu na Ikulu ya Watu, makao makuu ya Bunge, kuandamana hadi makao makuu ya Tume ya Uchaguzi (CENI).