Zoezi la kuhesabu kura linaendelea nchini Jamhuri ya Kidemokraisa ya Kongo siku sita baada ya kufanyika uchaguzi mkuu uliogubikwa na kashfa za wizi wa kura na kucheleweshwa kusambazwa vifaa vya uchaguzi.
Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi, CENI, Denis Kadima amesema tume hiyo haitosita kubatilisha baadhi ya matokeo ya uchaguzi iwapo udanganyifu utathibitishwa.
Kadima amesema vurugu zilizotokea siku ya uchaguzi hazikupangwa na CENI na amewatupia lawama baadhi ya wanasiasa ambao anasema walijaribu kuiba kura kwa kushirikana na baadhi ya mawakala wa tume ya uchaguzi.
Hadi Jumatatu 25.12.2023, baadhi ya maeneo yaliendelea kupiga kura, ikiwa ni siku tano baada ya uchaguzi kufanyika. Tume ya uchaguzi imesema hatua hiyo inalenga kuwapa fursa wapiga kura wote kwenye maeneo ambako vifaa vya uchaguzi vilichelewa kufikishwa tarehe 20 Desemba.
Kwa mujibu wa taarifa ya Tume ya Uchaguzi, CENI mpaka sasa kura milioni 1.9, zimeshahesabiwa kati ya jumla ya wapiga kura milioni 44 waliojiandikisha.
Rais Felix Tshisekedi anayewania muhula wa pili anaongoza kulingana na matokeo hayo ya awali. Tshisekedi anafuatiwa katika nafasi ya pili na Moise Katumbi aliyekuwa meya wa jimbo la Katanga, yeye pia ni mfanyabiashara mkubwa.
Wagombea wengine wapatao 20 ikiwa pamoja na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Denis Mukwege wameshindwa kufikia asilimia 1 ya kura za awali.