Uongozi wa Chama cha mpira wa miguu mkoa wa Pwani COREFA, umeanzisha bonanza la soka la wanawake kuanzia ngazi ya shule za Sekondari lengo ikiwa ni kuibua na kuviendeleza vipaji vya mabinti ambao watasaidiwa kutimiza ndoto zao.
Akizungumza juzi mkoani Pwani Mwenyekiti wa Chama hicho, Robert Munisi,wakati akiongea na Mabinti wa shule mbalimbali za mkoa wa Pwani ambazo zimeshiriki bonanza hilo kwenye uwanja wa Maliasili uliopo Halmshauri ya Mji wa Kibaha.
Alisema miongoni mwa vipaumbele vya mkoa huo ni kuinua soko la wanawake na katika kufanikisha hilo wanaandaa mabonanza ambayo yatawakutanisha ili kubadilishana uzoefu.
“Tuna mabinti wengi ambao wana vipaji vya kusakata kabumbu lakini kutokana na mazingira wanashindwa kuvionesha sasa COREFA tumeanzisha bonanza kwa ajili yao litakuwa endelevu kila shule za sekondari zitashiriki ili tuone uwezo wao na namna ya kuwasaidia,” alisema Munisi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Soka la Wanawake mkoani humo, Mariam Songoro, alisema mpira ni ajira na kwa sasa wanawake wana nafasi kubwa ya kupata fursa ndani na nje ya nchi.
Alisema soka ni ajira kama zilivyoajira nyingine ambazo zikiinua maisha ya watu hivyo wanatoa nafasi kwa mabinti hao kuonyesha uwezo wao.
“ Huu ni mwanzo tu mabinti zangu bonanza hili litawanufaisha sana, kazi yenu kubwa ni kujituma uwanjani, kufanya mazoezi, nidhamu ambayo itawafikisha kule mnapopataka lakini msisahau kusoma kwa bidii ili muwe na uwezo wa kuongea lugha mbalimbali mtakapoenda kwenye nchi za wenzenu kucheza soka,”alisema.