Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefunga mashine tatu za kusafisha damu kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo zenye thamani ya Tsh. Mil 210 na inatarajia kufunga mashine moja ya kusaidia mgonjwa kupumua (ventilator) yenye thamani ya TSh. Mil 56 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana ili kuhudumia wagonjwa wa corona. •
Tayari wagonjwa wanaohitaji huduma ya kusafishwa damu wameanza kuhudumiwa na wafanyakazi wa MNH waliopo Hospitali ya Amana tangu Ijumaa ya Aprili 24, 2020 saa 12 asubuhi ambapo dawa na vitendanishi vya kutoa huduma ya kusafisha figo kwa sasa vinagharimiwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili.
MNH pia imefunga mtambo wa kuchuja maji (Portable RO) wenye thamani ya Tsh. Mil 28 na mtandao wenye miundombinu ya kusafirisha maji ili kuwezesha mashine hizo kufanya kazi ya kusafisha damu uliogharimu Tsh. Mil 12.
MNH itapokea madaktari na wauguzi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Amana kuanzia April 28, 2020 ili kujengewa uwezo kwenye Kitengo cha Kusafisha Damu pamoja na vyumba vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICUs) aina tano tofauti.