NI Benki ya CRDB ambapo FEB 24,2021 imezindua huduma ya SimBanking iliyoboreshwa kuwawezesha wateja kupata huduma za kisasa na kufikia malengo yao ya kifedha.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo iliyoboreshwa na kupewa jina la ‘Benki ni SimBanking’, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Abdulmajid Nsekela, amesema inawawezesha wateja kuwa na uwanja mpana wa kupata huduma za kifedha kama vile kufungua akaunti kwa njia ya kidijitali, maombi ya mkopo, malipo ya bili na malipo ya bima.
“Kwa kupakua programu iliyoboreshwa ya SimBanking, mtu yeyote anaweza kufungua akaunti ya benki popote alipo bila gharama. Tunaamini programu hii mpya itachangia kuimarisha mfumo wa kifedha wa nchi yetu.
“Programu hii imeundwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa na tutajumuisha pia mfumo wa Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Tanzania (TIRA) ili kuwezesha wateja kupata stika za kidijiti kupitia programu hii mara baada ya kufanya malipo,” amesema Nsekela.
Naye Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndungulile, ameipongeza Benki ya CRDB kwa kubuni na kuanzisha bidhaa na huduma zinazoharakisha utekelezaji wa mipango ya kitaifa ya uchumi na maendeleo inayoendeshwa na serikali.
Dk. Ndugulile amewahimiza Watanzania hasa wale wa vijijini kutumia Programu ya SimBanking iliyoboreshwa kufungua akaunti za benki na kuanza kufurahia huduma za kibenki.
“Kwa kuwa sasa tuna njia rahisi ya kufungua akaunti ambayo haiitaji kutembelea tawi, naamini programu iliyoboreshwa ya SimBanking itatusaidia kujumuisha watu wengi katika mfumo rasmi wa kifedha,”amesema Dk. Ndugulile.