Leo August 4 2017 Mahakama Kuu ya Tanzania imetupilia mbali pingamizi la wabunge 8 waliotimuliwa na Profesa Ibrahimu Lipumba kupinga kuapishwa kwa wabunge wapya 8.
Katika uamuzi wake, Jaji Lugano Mwandambo amesema anatupilia mbali pingamizi la zuio la kuapishwa kwa wabunge hao 8.
Amesema sababu ya kulitupa pingamizi hilo ni kutokuwepo kwa kifungu sahihi kinachoyafanya maombi yao yawe sahihi mahakamani. Kwa mantiki hiyo, wabunge walioteuliwa na Lipumba wanaweza kuapishwa muda wowote.
Awali katika usikilizwaji wa pingamizi hilo, Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata alidai maombi hayo yamefunguliwa bila kuwekwa kifungu sahihi kinachoipa Mahakama mamlaka ya kusikiliza na kutoa uamuzi dhidi ya maombi hayo.
Amedai maombi hayo yamefunguliwa chini ya kifungu kidogo cha 2(3) ambacho kinaipa mamlaka Mahakama kutumia sheria ya Jumuiya ya Madola.
“Kama maombi hayo yameletwa chini ya kifungu hicho ilipaswa kiwepo kifungu husika kutoka katika sheria ya Jumuiya ya Madola, kisheria kinapaswa kutumika endapo hakutakuwa na sheria yeyote Tanzania inayozungumzia maombi hayo“.