Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Engineer Cyprian Luhemeja ametolea ufafanuzi sakata la ukosefu wa huduma ya maji safi katika maeneo mbalimbali ya jiji DSM nakusema hali hiyo imesababishwa na msukumo mdogo wa maji kutoka katika mitambo ya Ruvu Chini inayosafirisha maji kwenye makazi ya watu.
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekiri kupata taarifa za tatizo la upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo unaosababishwa na msukumo mdogo kutoka katika chanzo cha maji cha Ruvu Chini.
Luhemeja amesema kufuatia upungufu wa maji mtoni, uzalishaji wa Maji umepungua kutoka lita milioni 520 kwa siku hadi kufikia lita milioni 460. Upungufu huo unatokana na kupungua kwa uzalishaji katika mtambo wa Ruvu Chini ambao husambaza maji kwa asilimia 70 ya eneo la huduma la DAWASA. Mtambo wa Ruvu Chini kwa kawaida huzalisha lita milioni 270 kwa siku na hivi sasa unazalisha kiasi cha lita milioni 210 kwa siku.
“Kupungua kwa kina cha maji katika chanzo cha maji kumetulazimu kuhamisha maji kutoka Ruvu Juu ili kuhudumia baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakihudumiwa na mtambo wa Ruvu Chini,” Cyprian Luhemeja Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA
“Tuwaondoe wasiwasi, Dawasa tumejipanga na tuna maboza kwa wale ambao watakuwa na changamoto kubwa basi tutawapelekea maji, uzalishaji katika mtambo wa Ruvu Juu bado ni Lita milioni 127 kwa siku, Mtambo wa Wami pia unazalisha lita milioni 7.3 na chanzo cha mtoni pia kinazalisha lita milioni 6.8 hadi 7 kwa siku” Cyprian Luhemeja Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA