Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga, Jokate Mwegelo @jokatemwegelo amewataka Wafanyabiashara wanaoficha mafuta Wilayani Korogwe wakisubiria mabadiliko ya bei ili wauze kwa bei kubwa kuacha mara moja kwakuwa wanahujumu uchumi na pia wanaichafua Serikali.
DC Jokate amesema hayo leo July 31,2023 baada ya kutembelea Kituo cha Mafuta Mombo High Way ambacho hakijafanya kazi kwa siku ya tatu leo kwa kisingizio kuwa pump imeharibika “Kuna maeneo tunajua kuna changamoto lakini hapa mafuta mnayo leo siku ya tatu Wananchi hawapati huduma, hii haikubaliki”
“Tumejiridhisha kwa Mjini tuna akiba ya lita zaidi ya Laki 1.5, kuna Watu wanaficha mafuta wakisubiria mabadiliko ya bei, sasa kama Serikali hatuwezi kuruhusu Wananchi waumie kwasababu Mwekezaji hataki kutoa mafuta anasikilizia mabadiliko ya bei”
“Leo siku ya tatu mnaniambia mafuta hayapatikani kisa pump tu?, haiwezekani siku ya 3 hamjarekebisha pump , tunawaonya wanaoficha mafuta waache mara moja, tumefika Mombo High Way wana akiba ya mafuta zaidi ya Lita Elfu 10 ya petrol lakini leo siku ya 3 hawatoi mafuta na kisingizio chao pump imeharibika lakini tunajua wanasikilizia mabadiliko ya bei”
“Nimeongea na fundi wa pump, aje atengeneze na nitakuja tena usiku nikifika nataka nikute pump inafanya kazi Wananchi wanahudumiwa sitaki kukuta sababu, hatuwezi kukubali Serikali ichafuliwe kirahisi, kinachofanyika hapa ni kuichafua Serikali”