Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Njombe, Victoria Mwanziva ( @victoria.mwanziva ) kwa kushirikiana na Wafanyakazi wa Ofisi ya DC Ludewa wameamua kujinyima kwa kutolipana posho kwa miezi minne ili kuzitumia poshi hizo kufanya ujenzi na ukarabati wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambayo ilijengwa mwaka 1974 na majengo mabovu yaliyokuwa kama magofu yamekuwa yakitumika kwa kipindi chote hadi April 2024 bila kufanyiwa ukarabati.
Akiongea na @AyoTV_ ofisini kwake DC Victoria amesema yafuatayo….“Baada ya mwaka mmoja nikasema nina nafasi ya kuboresha Ofisi ya DC, nikasema nikisema nianze kumuomba Mh. Rais pesa kwa ajili ya kuboresha Ofisi na nikiwaza pesa alizoziingiza Ludewa kwenye miradi mbalimbali nikasema hapana tuna nafasi ya kujibana kama Ofisi ya DC kuboresha Ofisi, tuna fedha za kuendesha Ofisi tukajibana kwa miezi minne bila kulipana posho wala kutumia fedha zozote za maendesho ya Ofisi kwa ajili ya Ofisi yetu , tukapata kibali cha RC na RAS na kuboresha ofisi”
“Mh. Rais anasema tubane matumizi tuoneshe pesa yetu tunaweza kuitumia ikatosha ndio tulichotaka kuonesha kwamba Wilaya ya Ludewa tunaweza kitu kidogo kikachipua kuwa kikubwa kwa kujibana na kusimamia, tumetumia zaidi ya milioni 20 na TARURA wametusaidia vifaa mchanga, kokoto na baadhi ya vifaa”
“Hapa ofisini tuna gari moja tu la DC ndio tunatumia Ofisi nzima, lile sio gari langu ni gari la Umma hata sisi hivi lipo kwenye kazi, nyumba ya DC nayo ni ya mwaka 1975 maboresho na ukarabati unaendelea na unasimamiwa na Ofisi ya RC”