Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mobhare Matinyi, amekabidhi bendera ya Taifa kwa Vijana saba wa Temeke ambao wamejitolea kutembea kwa miguu wakizunguka Mikoa 16 kutangaza kazi alizofanya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Wilayani Temeke.
Akiwakabidhi bendera ofisini kwake, DC Matinyi amezitaja baadhi ya kazi zilizofanywa Temeke mwaka 2022/23 na thamani ya fedha zilizotolewa na Rais Samia kuwa ni pamoja na miradi ya afya sh. bilioni6.1, elimu ya msingi sh. bilioni 7.6, elimu ya sekondari sh. bilioni 10, maji sh. bilioni 15.5, umeme sh. bilioni 61.6 na barabara sh. bilioni 43.7.
Amesema Vijana hao Wazalendo wameondoka Dar es Salaam leo asubuhi kuanza matembezi katika Mikoa 16 huku akisema kwa ujumla Temeke ilipatiwa na Rais Samia zaidi sh. bilioni 152 katika kipindi hicho kutokana na wingi wa Wakazi wake ambao wanafikia milioni 1.35 na nia yake ya kuleta maendeleo kwa Watanzania.
Amewaambia Vijana hao kuwa katika kilomita 3,624 wanazotarajia kutembea kwa miguu watakutana na ushahidi lukuki wa kazi za Rais Samia, Vijana hao saba wanaoongozwa na Abihudi Maugo wanatarajiwa kuhitimisha matembezi yao Mkoani Manyara wakati wa sherehe za kuuzima mwenge October 14, 2023.
Vijana wengine ni Sophia Kooni, Beatrice Masanja, Shabani Juma, Jesca Giribert, Flora Erenest na Paul Mkinga, hii ni mara ya nane kwa Vijana wa Temeke kufanya matembezi nchini kuunga mkono matukio au dhima tofauti.