Leo October 10, 2018 Serikali imepiga marufuku Madaktari kuwaandikia wagonjwa Dawa kwa kutumia jina la Kampuni kwani Serikali haifanyi biashara hivyo wanatakiwa kutumia majina ya Kitaalam.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dr. Faustine Ndugulile amezungumza hayo katika Mkutano wa Tanzania Health Supply Chain Summit kwa mwaka 2018 ambapo amewata watumie majina ya kitaalamu.
Dr. Ndugulile amesema tabia ya kutumia majina ya kampuni kumesababisha Wagonjwa kukosa dawa licha ya kuwapo kwa dawa nyingine zenye uwezo wa kutibu sawa na hizo
“Dawa zinazotumika hapa nchini ni sawa na zile zinazotumika katika nchi nyingine duniani kwa hiyo kutoa dawa China, India, Marekani au Ulaya ni utofauti wa gharama.” -Dr. Ndugulile
“Mfano mimi ni daktari nikikuandikia ukanunue soda ukikuta soda yoyote utapona ila nikikwambia ukanunue Cocacola lazima uipate hiyo.” -Dr. Ndugulile
Nae Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Dkt. Zainabu Chaula amesema kuwa ni vyema madaktari wakazingatia maagizo yale yote ambayo yamekuwa wakitolewa na viongozi.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Laurean Bwanakunu amesema kuwa wao wamejipanga na wanaakiba ya kutosha ya dawa hivyo ni vyema wahusika kufuata utaratibu ili wanunue na wapelekewe kwa wakati muafaka.
Kongamano la Wadau wa Mnyororo wa Ugavi wa Dawa- Tanzania (Tanzania Health Supply Chain Summit 2018) linawakutanisha wadau wote wa masuala ya afya kutoka nchi nzima.