Mfuko wa DEEP Challenge Fund Tanzania, umezinduliwa hii leo Machi 22, 2024, ukiwa unalenga kuboresha mkakati wa kitaifa, sera, na programu zinazoathiri umaskini na mazingira magumu ya umaskini nchini Tanzania, kwa kufadhili watafiti na wachambuzi wa kitaifa ili kutoa maarifa na ushahidi unaoendana na mahitaji ya watunga sera.
Mfuko wa DEEP Challenge Fund ulilenga Tanzania kuwa nchi ya kwanza kutokana na changamoto zake kubwa za kupunguza umaskini, tamanio na hitaji la ushahidi wa kitafiti na mabadiliko ya sera. Mfuko huu utaanza kutumika nchini Bangladesh na Nigeria baadaye mwaka huu. Mtazamo wa utafiti, malengo na upeo wa Mfuko wa Changamoto Tanzania unaundwa na watunga sera wa Tanzania na wadau wengine wakuu.
Kamati ya Uongozi ya wawakilishi wa serikali ya Tanzania, wasomi, mashirika yasiyo ya kiserikali na watu wengine imezindua mfuko huu Machi 22 katika warsha itakayofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Maombi ya ufadhili wa mfuko huu yatafunguliwa baada ya kufanyika kwa warsha. Ufadhili mdogo na wa kati utatolewa kwa mashirika na/au watu binafsi kufuatia mchakato wa ushindani wa zabuni.
Mapendekezo ya kiutafiti yanayohimizwa ni yale ambayo yatasaidia kutoa maarifa mapya kuhusu vichochezi vya umaskini – kama vile mabadiliko ya tabia ya nchi, UVIKO, ukuaji wa miji, uhamiaji, migogoro, Unyanyapaa wa jamii, na desturi za kijamii – au uchambuzi juu ya ‘nini kinafaa?’ kuhusiana na sera za serikali na programu zinazojumuisha malengo ya kupunguza umaskini.
Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Sera ya Oxford Ofisi ya Tanzania na Mwenyekiti mwenza wa Kamati ya Uongozi ya Taifa ya DEEP Dk. Charles Sokile alisema.
“Ni wakati wa kusisimua nchini Tanzania, mpango mkakati wa maendeleo ya Dira ya 2050 ni fursa ya mara moja kwa kizazi kuunda mustakabali wa nchi yetu. Na kwa hivyo, data na uthibitisho kuhusu njia bora zaidi na za kudumu za kuweza kukabiliana na umaskini zitakuwa na jukumu muhimu katika kuunda dira ya nchi.”Dk Sokile aliongeza,
“Tunazindua Mfuko mpya wa DEEP Challenge Fund kusaidia watafiti nchini Tanzania ili kukidhi hitaji hili la uthibitisho, na hatimaye kuboresha maisha ya watu wanaoishi katika umaskini.”