Kiwango cha deni la Kenya kimefikia kiwango cha juu licha ya kiapo cha Rais William Ruto cha kupunguza hamu ya mikopo ya nchi hiyo, takwimu za hazina zinaonyesha.
Jumla ya deni la umma lilipanda kwa rekodi ya shilingi trilioni 1.56 (dola bilioni 10.8) katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30 hadi shilingi trilioni 10.1 (dola bilioni 70.75), na kukiuka ukomo wa deni la shilingi trilioni 10, kulingana na data iliyotolewa Jumanne.
“Ongezeko la deni la umma limechangiwa na utoaji wa mikopo ya nje, kushuka kwa kiwango cha ubadilishaji fedha na kulipwa kwa deni la ndani na nje,” Hazina ilisema.
Deni la taifa lilipanda kwa asilimia 18%, na kupita dola bilioni 69.52 ambazo Kenya inafaa kukopa kwa mjibu wa katiba.
Hata hivyo mwezi Juni bunge la Kenya lilipitisha mwaswada unaoruhusu serikali kukopa angalau asilimia 55% ya pato la taifa kikiwa ni kiwango cha juu zaidi cha deni ikilinganishwa na ilivyokuwa awali.
Gharama ya kulipa deni katika mwaka ulioishia Juni ilikuwa shilingi bilioni 391 (dola bilioni 2.7), ambapo malipo ya juu zaidi — shilingi bilioni 107 (dola milioni 743) yalikwenda China.
Wingi wa deni umesababisha maonyo kutoka kwa mashirika ya kimataifa ya kutathmini viwango vya mikopo ikiwa ni pamoja na Fitch Ratings ambayo mwezi uliopita ilishusha uwezo wa Kenya wa kulipa wakopeshaji wa kimataifa kutoka “imara hadi hasi”, ikitaja ongezeko la ushuru na machafuko ya kijamii.
Wabunge wa Kenya walipiga kura mwezi Juni kubadilisha kiwango cha juu cha deni kutoka kiasi cha shilingi kilichopangwa hadi sehemu ya pato la taifa (GDP). Seneti bado haijapitisha marekebisho hayo.
Ruto aliingia mamlakani mwaka jana kwa ahadi ya kufufua uchumi katika nchi hiyo yenye takriban watu milioni 53.