Winga wa Argentina Angel Di Maria ameachana na Juventus baada ya msimu mmoja, na kuwa mchezaji huru huku kukiwa na madai kuwa anaweza kulengwa na klabu moja nchini Saudi Arabia.
Mshindi huyo wa Kombe la Dunia mwenye umri wa miaka 35 alifika Turin baada ya misimu saba akiwa na Paris Saint-Germain, akifunga mabao nane katika mechi 40 alizoichezea Juve katika msimu usio na taji lolote.
“Naondoka nikiwa na amani ya akili kwa kujitolea kila kitu kusaidia klabu kuendelea kushinda mataji, lakini haikuwezekana,” Di Maria alisema kwenye Instagram.
“Ninaondoka nikiwa na uchungu wa kutofanikisha hilo, lakini pia nikiwa na furaha ya kuchukua pamoja nami marafiki wengi kutoka kwenye chumba kizuri cha kubadilishia nguo ambacho nilikuwa sehemu yake.”
Saudi Arabia imeandaa orodha ya wachezaji zaidi ya 10 ambao wameshinda Ligi ya Mabingwa au Kombe la Dunia ambayo inataka kuwavutia kwenye ligi yake, chanzo kilicho karibu na mazungumzo hayo kimeiambia AFP.