Baada ya tetesi za muda mrefu zikimhusisha na kuihama klabu ya Manchester United baada ya msimu mmoja ambao umeonekana si wa mafanikio sana, kiungo raia wa Argentina Angel Di Maria amethibitisha kuwa ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Manchester United msimu ujao.
Di Maria amekuwa kwenye wakati mgumu katika msimu wake wa kwanza baada ya kuonekana amecheza chini ya kiwango katika msimu ambao United imemaliza kwenye nafasi ya nne na kufanikiwa kufuzu michuano ya ligi ya mabingwa ambayo waliikosa msimu uliopita.
Pamoja na kauli nyingi za wachambuzi na mashabiki kumfanya aonekane amecheza chini ya kiwango bado Di Maria ameweza kutimiza idadi ya mabao manne na pasi 12 za mwisho akiwa moja ya wachezaji ambao wametoa pasi nyingi za mwisho.
Di Maria ambaye alisajiliwa kwa paundi milioni 55 akitokea klabu ya Real Madrid alianza msimu kwa kasi kabla ya kupotea baada ya kupata majeraha huku akiathirika kisaikolojia baada ya nyumba yake jijini Manchester kuvamiwa na majambazi.
Mchezaji huyo mwenyewe amekiri kuwa kuzoea mazingira ya ligi ya England imekuwa vigumu kuliko alivyotarajia hapo awali na ameahidi makubwa zaidi kwenye msimu ujao ambao utakuwa msimu wake wa pili .
Di Maria kwa sasa yuko kwenye kambi ya timu ya taifa ya Argentina ambako anajiandaa na michuano ya kombe la mataifa ya Amerika ya Kusini maarufu kama Copa America .