Serikali kupitia Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) ikishirikiana na Kampuni ya ujenzi ya Group Six international imetoa ufadhili wa miaka miwili wa Wanafunzi 30, wa Kada ya Uhandisi Majengo kwenda nchini China kwa ajili ya kupata mafunzo katika Chuo cha ChonqQhing Vocational Institute of Engineering.
Bi, Chen Ming Jiang, ambaye ni Balozi wa China nchini Tanzania alisema hayo wakati akiwaaga wanafunzi hao na kuwaeleza kuwa sera bora na mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na amani ndio kitu pekee ambacho wawekezaji wanataka katika nchi ambazo zinazoendelea,
Aidha, balozi huyo alisema kuwa kutokana na uwepo wa mazingira mazuri ya uwezekaji na ndiyo maana kampuni ya group six international kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia wamekubali kuwapeleka wanafunzi hao kwenda kujijengea uwezo katika taaluma yao ya uhandisi majengo kwani nchi ya China iko mbele kwenye teknolojia ya uhandisi na ni ndoto ya vijana wengi wa Afrika kutaka kwenda kusoma Nchini China.
Balozi, Chen Ming Jiang amewasihi wanafunzi hao kutumia vyema ufadhili huo kwa kusoma nchini China vizuri kwani licha kuwa watakabiliwa na mazingira tofauti wakiwa nchini humo bali pia waongeze bidii na juhudi kubwa katika kuzingatia masomo yao na kile kilichowapeleka nchini humo.
Aidha, alisema kuwa utofauti wa mazingira, chakula na utamaduni ni vitu ambavyo ana uzoefu navyo na kuwataka wanafunzi hao kuweka utayari kwa kusoma ili wakirudi nchi waweze kusaidia kuleta maendeleo na kuwataka kukabiliana nayo mazingira mapya.
Pia, balozi huyo amewataka wanafunzi hao kuwa mabalozi bora kwa muda wote watakapokuwa nchini China kwani nchini hizi mbili kati ya Tanzania na China zina mahusiano mazuri toka kipindi kirefu.
“Urafiki wa Tanzanian na china ulianza pale China ilipojenga Reli ya Tazara na jambo lingine la kihistoria ni kwamba Rais wa Sita wa Tanzania Dr Samia Suluhu Hassan, kwa mwaka huu mmoja amekutana na Rais wa Jamhuri ya watu wa China mara mbili. kukutana mara mbili ya kwanza ikiwa ni ziara aliyofanya nchini China kwa mwaliko wa Rais Xhi Ji Pin na mara ya pili walikutana mwenye mkutano wa Brix’’, alisema balozi huyo.
Kwa upande wake Amani Kakana, Mkuu wa kitengo cha habari na uhusiano wa DIT alieleza kuwa, Taasisi hiyo kwa mara ya kwanza imetoa wanafunzi hao, baada ya serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kuingia mkataba wa ushirikiano wa miaka 5 na Chuo cha ChonqQhing Vocational Institute of Engineering cha nchini China kwa wanafunzi kwenda kusoma katika chuo hicho..
Mkuu huyo wa mahusiano alisema kuwa mkataba uliosaniwa kati ya Chuo cha ChonqQhing Vocational Institute of Engineering na DIT ni kuweza kuwasaidia Waandisi Vijana wa Kiafrika kuweza kupata ujuzi wa viwango ambavyo kampuni nyingi za ujenzi kutoka China wanataka wawenavyo.
“Katika mkataba huo kipo kipengele kinaelekeza uwepo wa wigo wa ajira kwenye sekta ya ujenzi, ambavyo vitaendana na kupunguza ajira ambazo sio rasmi na kuongeza thamani kwa waandisi wanaochipukia kuendana na soko la ajira katika ujenzi” alisema Kakana.