Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo ameshuhudia uwekaji saini Mkataba wa Mauziano ya Gesi Asilia itakayozalishwa katika eneo la Ntorya Kitalu cha Ruvuma na uwekaji saini hati ya Makubaliano kwa ajili ya kuanzisha mahusiano ya kujenga miundombinu ya kusambaza Gesi Asilia kwa Teknolojia ya miundombinu midogo ya kubadilisha Gesi Asilia kuwa kimiminika (Mini-LNG).
Hafla ya utiaji saini imefanyika tarehe 10 Januari, 2024, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo Mkataba wa Mauziano ya Gesi Asilia itakayozalishwa eneo la Ntorya umesainiwa kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kampuni ya ARA Petroleum ya Oman na Ndovu Resources ya Uingereza.Hati ya Makubaliano kwa ajili ya kuanzisha mahusiano ya kujenga miundombinu ya Gesi Asilia imesainiwa kati ya TPDC na Kampuni ya KS Energy.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Biteko amesema kuwa, Mkakati wa Wizara ya Nishati ni kuhakikisha kuwa inasimamia ipasavyo Sera ya Nishati ya mwaka 2015 na kuhakikisha kuwa kunakuwa na upatikanaji wa nishati safi ambayo itawafikia wateja mbalimbali kwa urahisi na bei nafuu.
Amesema kuwa, lengo la nchi ni kuwa na nishati inayotokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo Jua, Upepo, Gesi na Maji ili Gesi Asilia iliyopo itumike pia kwa kiasi kikubwa kwenye maeneo mengine kama viwanda na majumbani badala ya kutumika kwa kiasi kikubwa kwenye umeme na pia kupunguza matumizi ya mafuta.
“Mkakati wetu ni kubadilisha suala hili la Gesi Asilia kutumika zaidi kwenye umeme ambayo ni takriban asilimia 80, tunataka kuwe na nishati mchanganyiko nchini ili gesi itumike kwenye viwanda na majumbani na pia tupunguze utegemezi wa mafuta.” Amesema Dkt. Biteko
Kuhusu Hati ya Makubaliano kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu midogo ya kubadilisha Gesi Asilia kuwa kimiminika (Mini-LNG), ameeleza kuwa, mradi utakuwa wa kwanza kufanyika nchini na utawezesha kupunguza kiu ya watanzania kutumia Gesi Asilia hata kwa maeneo yaliyo mbali na miundombinu ya mabomba na hivyo kuchochea matumizi ya nishati safi nchini.
Hafla hiyo ya utiaji saini makubaliano imehudhuriwa pia na Wabunge Mkoa wa Mtwara, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mohamed Fakihi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue na Menejinenti ya TPDC.