Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb) Dkt Jafo ameiagiza Wakala wa Vipimo (WMA) kukamilisha utaratibu wa kupima mita za umeme na mita za maji kabla hazIjafungwa kwa wateja ndani ya mwezi mmoja ili kulinda haki za walaji.
Dkt. Jafo ameyasema hayo alipotembelea WMA katika Kituo cha uhakiki wa vipimo Misugusugu Mkoani Pwani.
Dkt Jafo ameiekekeza Wakala hiyo kuwalinda wakullima wa mazao mbalimbali kuuza mazao yao kama vile pamba katika vipimo sahihi hususani kwa kudhibiti lumbesa ili wapate haki yao sawasawa na ujazo sahihi wa mazao yao.
“Suala la vipimo ni Ibada hata vitabu vyote vya Dini vimeeleza kuwa kila bidhaa inayouzwa iwe katika vipimo sahihi bila kumhujumu mlaji. Hivyo WMA tuwahamasishe wananchi hususani wakulima kuacha kukadria mazao bali watumie vipimo sahihi wanapouza au kununua bidhaa ili wapate haki yao wanaostahili” Alisisitiza Dkt Jafo.
Vilevile ametoa wito kwa wazalishaji saruji pamoja na vifaa vingine vya ujenzi kuhakikisha kuwa vinakuwa katika vipimo sahihi kulingana na ujazo uliotajwa ili kuwalinda wafanyabiashara na walaji wa bidhaa hizo kwa kupata bidhaa zinazolingana na thamani yake.