Waziri wa Ulinzi na JKT, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) ameongoza wageni waalikwa wakati wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Majeshi ya Misri. Maadhimisho ya Siku ya Majeshi huadhimishwa nchini humo kila ifikapo tarehe 06 Oktoba ya kila mwaka, kufuatia ushindi yaliyoupata wakati wa vita ya Misri ikisaidiwa na Syria dhidi ya majeshi ya Israeli tarehe 06 Oktoba, 1973, ushindi uliwawezesha kuukalia mlima Sinai.
Maadhimisho hayo hapa nchini yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Misri hapa nchini yameadhimishwa leo tarehe 12 Oktoba, 2023 katika hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.
Akihutubia wageni waalikwa katika hafla hiyo, Mheshimiwa Dkt. Stergomena ametoa pongezi kwa majeshi ya Misri, Serikali, na wananchi wa misri kwa ujumla, katika kuadhimisha siku hii muhimu.
Aidha, Mheshimiwa Waziri amewashukuru kwa heshima waliyompa ya kuwa Mgeni Rasmi katika tukio hilo muhimu ya kuadhimisha siku muhimu kwa taifa hilo.
Ameongeza kusema kuwa mwaliko huo, ni kielelezo tosha kuwa ushirikiano wa vmuda mrefu na wa kihistoria, uliopo baina ya watu wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri na watu Jamhuri ya Muungano wa Tanzzania.
Vile vile, Mheshimiwa Dkt. Stergomena aliwasilisha salamu za pongezi na za kuwatakia kila la kheri katika kuadhimisha siku hii muhimu kwa taifa la Misri, kutoka kwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akibainisha umuhimu wa siku hii, Dkt. Stergomena amesema kuwa kuadhimishwa kwa siku hii, kunatukumbusha ari, ujasri na kujitoa kwa majeshi hayo katika kulinda taifa lao, utu wao pamoja na kuimarisha utulivu wa taifa lao. Ameongeza kusema kuwa maadhimisho ya mwaka huu si tu kwamba yanaonesha mafanikio ya majeshi haya, bali pia inatoa fursa ya kuimarisha urafiki baina ya mataifa haya mawili, kwani kupitia ushirikiano huu kutaimrisha zaidi usalama wa pamoja na ustawi wa mataifa haya mawili na dunia kwa ujumla.