Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) ambaye pia ni Spika wa bunge la Tanzania na Mbunge wa Mbeya Mjini Mhe. Dkt.Tulia Ackson, amewatolea uvivu baadhi ya watu wanaomuandama mitandaoni kuwa anawatangaza watu anaowapa misaada ambapo ameeleza kuwa anafanya hivyo ili kutoa funzo kwa wengine kuiga mfano wa kuwasaidia wahitaji.
Dkt.Tulia ametoa kauli hiyo tarehe 22 Januari,2024 wakati alipoiongoza taasisi ya Tulia Trust kutoa msaada wa sare za shule na madaftari kwa wanafunzi 3000 wa shule za msingi wanaoishi kwenye mazingira magumu Jijini Mbeya.
Dk.Tulia amesema wapo baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii ambao wanamshukia kuwa hapaswi kuwatangaza watu ambao wanapewa misaada na taasisi yake au yeye binafsi.
Amesema anafanya hivyo ili kutoa funzo kwa wengine kutambua wajibu wao wa kuwasaidia watu wanaoishi kwenye mazingira magumu, akitoa wito Kwa jamii kuwa na utamaduni wa kujitolea Kwa watoto ambao wanapitia changamoto za maisha kutokana na hali duni za maisha.
“Mahitaji haya yanawahusu wanafunzi wa darasa kwanza hadi la nne wanaotoka kwenye familia zenye changamoto,sisi pia tuna hilo jukumu ya kusaidia wengine anza na jirani yako asilale njaa, usisubiri uwe na kikubwa hicho hicho ulicho nacho kinatosha,”amesema.
Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kiwango kikubwa imeboresha miundombinu ya elimu katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya ikiwemo kujenga matundu ya vyoo zaidi ya 310.
Hata hivyo amesema kazi ya kuboresha sekta ya elimu ni endelevu na inagusia maeneo mengi ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na shule kwenye maeneo ambayo hayana huduma ya elimu.