Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amewataka Wananchi wa Jimbo hilo kumshukuru sana Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele katika kuwaletea maendeleo ya haraka katika kipindi kifupi cha Uongozi wake.
Dkt. Tulia amesema hayo leo tarehe 14 Agosti, 2023 akiwa katika Mkutano wa hadhara na Wananchi wa Kata ya Itiji iliyopo Jijini humo ambapo amewaeleza kuwa katika kipindi cha miaka miwili na nusu pekee Serikali kwa kushirikiana naye wameweza kufikisha huduma nyingi za kimaendeleo ambazo hazijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa Jimbo hilo.
Akitoa mfano huduma hizo ni pamoja na ujenzi wa Zahanati na Vituo vya afya kila Kata, kuanza kwa ujenzi wa barabara ya njia nne pamoja na za mitaa kwa kiwango cha lami, ujenzi wa shule za Msingi na Sekondari kila Kata, kuboresha huduma za umeme na maji n.k
Ameongeza kuwa kupitia taasisi yake ya Tulia Trust amekuwa na utaratibu wa kila mwaka kutoa bima za afya bure kwa watu wasio na uwezo ambapo kwa mwaka jana alitoa bima 6000 pamoja na kutoa mitaji bure kwa wakinamama Wajasiriamali wa Jimbo lake.