Habari ya Asubuhi!Karibu kwenye Matangazo yetu hii leo Jumanne 15.8.2023
Donald Trump ameshtakiwa huko Atlanta (Georgia), na baraza kuu la mahakama kwa kujaribu kutengua matokeo ya uchaguzi wa rais wa 2020 katika jimbo la Marekani la Georgia, hasa kwa kuweka shinikizo kwa maafisa wa uchaguzi. Hili ni shtaka la nne kwa rais huyo wa zamani kutoka chama cha Republican, ambaye anagombea tena kwenye kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka 2024.
Uamuzi huo ulichelewa kutolewa baada ya kesi hiyo kudumu siku nzima siku ya Jumatatu katika mahakama huko Atlanta, anaripoti mwandishi wetu hko New York, Loubna Anaki.
Wakati huu, rais huyo wa zamani anatuhumiwa kwa udanganyifu na kuingilia uchaguzi huko Georgia, jimbo kuu ambalo alishindwa mnamo mwaka 2020 na Joe Biden. Kwa sasa Donald Trump anakabiliwa na mashtaka kumi na matatu.
Na hayuko peke yake, karibu washirika ishirini wa karibu pia wanalengwa na mashtaka haya. Miongoni mwao, Rudy Giuliani, wakili John Eastman, na Marc Meadows, mkuu wa zamani wa wafanyakazi wa Donald Trump.