Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), amefanya mabadiliko katika kesi ya uhujumu uchumi ambayo ilikuwa na mashtaka Tisa inayowakabili waliokuwa watumishi wanne wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ( NEMC).
DPP alifanya mabadiliko ya kuwafutia shtaka moja la utakatishaji fedha leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi na kisha kuwasomea upya mashtaka manane yakiwemo kuisababishia hasara Baraza hilo Sh.Mil 18.5
Washtakiwa hao ni Deusdedith Katwale, Magori Matiku, Obadia Machupa ambao ni Maofisa Mazingira wa NEMC na Mhasibu Msaidizi wa baraza hilo, Lydia Nyinondi ambapo walisomewa mashitaka na Mwendesha Mashitaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU), Nickson Shayo.
Miongoni mwa mashtaka, wanadaiwa kula njama ya kughushi, kutoa nyaraka za uongo na kuisababishia hasara Mamlaka hiyo kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Juni mosi mwaka 2016 na Julai 30, mwaka 2017 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na Dodoma.
Shtaka jingine linalomkabili Katwale, ambapo inadaiwa kati ya Agost 2, mwaka 2016 na Septemba 6, mwaka 2016 katika Ofisi za Nemc zilizopo Kinondoni, Dar es Salaam, mshitakiwa alighushi ya ripoti ya mradi wa ujenzi wa kituo cha mafuta cha Ibra General Enterprise Fuel Filling Station iliyopo kitalu T, kiwanja namba 132 kilichopo eneo la Chadulu Area A, mkoani Dodoma, akionyesha kuwa tathimini ya Mazingira katika mradi huo imefanyika , jambo ambalo sio kweli.
Pia Katwale anadaiwa kughushi nyaraka akionyesha kuwa kulifanyika mhutasari wa kikao cha kiufundi cha tathimini ya mazingira katika mradi huo, jambo ambalo sio kweli.
Pia shtaka la matumizi mabaya ya madaraka linawakabili washtakiwa wote, inadaiwa kuwa wakiwa Watumishi wa NEMC, walikiuka kifungu cha sheria ya mazingira kwa kufanya matumizi mabaya na kujipatia sh. milioni 18.5
Baada ya kuwasomea mashitaka hayo, washitakiwa walikana na upande wa mashitaka walidai upelelezi haujakamilika kisha kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Shaidi alitaja masharti ya dhamana kuwa kila mshitakiwa awe na mdhamini mmoja mwenye kitambulisho cha Taifa atakayetia saini dhamana ya Sh.Mil 20.
Hata hivyo, mshitakiwa Machupa alishindwa kudhaminiwa kwani inadaiwa ana kesi mengine nje ya Dar es Salaam, huku wengine wakikamilisha masharti na kuachiwa kwa dhamana.