Mvutano umekuwa ukiongezeka kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na nchi jirani ya Rwanda huku kukiwa na mapigano makali mashariki mwa DRC, ambayo Umoja wa Mataifa unasema yanazidisha matatizo ya rasilimali ambazo tayari ni chache za kuwahudumia wakimbizi wa ndani 800,000 katika eneo hilo na milioni 2.5 waliokimbia makazi yao katika jimbo la Kivu Kaskazini.
Jumamosi, jeshi la DRC kupitia msemaji wake Ndike Kaiko, liliishutumu Rwanda kwa kufanya shambulio la droni kwenye uwanja wa ndege wa Goma, mji mkuu wa Mkoa wa Kivu Kaskazini, ambako mapigano yamekuwa yakiendelea kati ya vikosi vya serikali ya DRC na makundi ya waasi wenye silaha, hasa wa M23.
Hata hivyo Rwanda bado haijajibu shutuma za DRC kuhusu shambulio hilo, lakini katika taarifa yake ya Jumapili, Rwanda iliishutumu serikali ya DRC kwa “kutelekeza Mchakato wa Luanda na Nairobi” na kulalamikia “jumuiya ya kimataifa kutojali ujenzi mkubwa wa kijeshi wa DRC”.