Siku sita baada ya vifo vya wafungwa wasiopungua 129 walipokuwa wakijaribu kutoroka katika gereza kubwa la Makala nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakati umefika wa kuwahesabu wahanga. Matokeo bado hayajafahamika kwani utambuzi wa wafungwa wakiwemo waliofariki ni wa muda mrefu na mgumu.
Nchini DRC, kumbukumbu za gereza la Makala mjini Kinshasa zikiwa zimechomwa moto, mamlaka inatarajia kutambua maelfu ya wafungwa mmoja baada ya mwingine katika gereza hili. Familia za waliofariki katika mkasa huu zimealikwa kuwatambua wapendwa wao.
Viongozi bado wanataja vifo vya watu 129, waliopigwa risasi na vikosi vya usalama, au kukosa hewa au kukanyagwa wakati wa machafuko yaliyotokea kwenye gereza la Kinshasa usiku wa Septemba 1 kuamkia Septemba 2. Hata hivyo, hakuna wafungwa walioripotiwa kutoroka. Tume ya usalama kati ya idara imeundwa kuchunguza mkasa huu.
Mchakato ambao utachukua muda, huku baadhi ya wafungwa wakitoka mikoa jirani, wengine wakiwa gerezani kwa miaka mingi na wamepoteza mawasiliano kabisa na familia zao. Tangu siku ya Alhamisi, Septemba 5, kesi pia imefunguliwa dhidi ya karibu wafungwa thelathini wanaoshtakiwa kwa ubakaji na uharibifu wakati wa jaribio hili la kutoroka huko Makala.