Rais Felix Tshisekedi amesistiza kuwa serikali yake haitafanya mazungumzo yoyote ya kisiasa na waasi wa M23, ambao Kinshasa inaseama wanaungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda
Tshisekedi aliyasema haya wakati wa mkutano wa pamoja kwa vyombo vya habari na mgeni wake rasi wa Uswizi, Alain Berset, ambaye yuko ziarani nchini humo.
“Hapa hakuna suala la majadiliano na kundi hilo, ninasema na kuweka wazi kwamba hilo halitatokea kwa sababu wanaoyumbisha usalama wetu tunafahamu mbinu wanazotumia.”ameeleza rais Tshisekedi.
DRC imekuwa ikiituhumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaotekeleza mashambulio ya raia katika eneo la mashariki ya taifa hilo madai ambayo Kigali kwa upande wake imeendelea kukana.
Kwa upande wake rais Berset, amesema nchi yake iko tayari kuisaidia DRC kwa kuhakikisha suala la nchi hiyo kuvamiwa na jirani zake ikiwemo Rwanda, kwa mujibu wa ripoti ya umoja wa mataifa, linafika katika ngazi ya kimataifa na baraza la usalama la umoja wa mataifa.
M23 pia wametuhumiwa kuendelea kutekeleza mashambulio ya raia licha ya kutakiwa kusisitisha mapigano kwa mujibu wa makubaliano ya Luanda Angola.
Tayari wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika mashariki wametumwa nchini Jamhurui ya Kidemokrasia ya Kongo kuwakinga raia kutokana na mashambulio ya makundi ya watu wenye silaha haswa mashariki ya taifa hilo.
Rais Felix Tshisekedi ameendelea kusisitiza kuwa serikali yake haitafanya mazungumzo na makundi ya kigaidi haswa M23.