Kampeni kuelekea uchaguzi wa mwezi ujao nchini DRC, zilizinduliwa rasmi mwishoni mwa juma lililopita, ambapo wagombea 26 wanawania kiti cha urais na baadhi walizindua kampeni zao hapo jana Jumapili, katika uchaguzi ambao unatazamwa kwa karibu na jumuiya ya kimataifa.
Rais wa sasa Felix Tshisekedi anayewania kuchaguliwa kwa muhula wa pili, alizindua kampeni zake hapo jana jijini Kinshasa kwenye uwanja wa Martyrs, ambapo aliahidi kukamilisha ahadi za uchaguzi na kusimamia usalama mashariki mwa nchi hiyo.
Mwingine aliyezindua kampeni zake hapo jana Jumapili ni Martin Fayulu, ambaye alikuwa kwenye mji wa Bandundu, alikoahidi raia uwa atashughulikia changamoto zinazoikabili nchi kwa sasa, huku muwaniaji mwingine Delly Sesanga, akianza kampeni zake katika mkoa wa Kwango, wakati Seth Kikuni na Jean-Claude Baende wakianza kampeni yao huko Kinshasa.
Tume ya uchaguzi CENI imewataka wawaniaji kufanya kampeni za kistaarabu, wakati huu jumla ya wagombea zaidi ya laki moja wakiwania nafasi mbalimbali ikiwemo, ubunge, useneta, ugavana na wawakilishi.
Ni kampeni zinazotazamwa si tu na raia wa Congo lakini jumuiya ya kimataifa na waangalizi wa uchaguzi, ambao wametoa wito wa amani licha ya eneo la mashariki kukabiliwa na utovu wa usalama, hali inayozua maswali ikiwa baadhi ya maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo yatafanya uchaguzi.