Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Patrick Muyaya amesema matokeo ya uchaguzi wa wiki jana wa Urais unaotiliwa shaka na upizani hayatabatilishwa licha ya wito wa mara kwa mara kutolewa na upinzani kutaka uchaguzi huo urudiwe.
Matokeo yaliyotolewa kufikia sasa kufuatia uchaguzi wa Desemba 20 yanamuonyesha Rais Felix Tshisekedi akiongoza dhidi ya wapinzani wake. Mvutano hata hivyo unaongezeka kuhusu uchaguzi huo ambao unatishia mukstkabal wa taifa la DRC, ambalo bado linakabiliana na mzozo wa usalama katika maeneo ya mashariki. Kongo ndio mzalishaji mkuu wa cobalti, vyuma, na madini mengine ya kiviwanda.
Maafisa wa usalama waliwakabili waandamanji na kuzima maandamano yaliyopigwa marufuku siku ya Jumatano katika mji mkuu Kinshasa na watu waliokuwa wakipinga jinsi uchaguzi wa rais na wabunge ulivyoendeshwa. Upinzani umesema kulikuwa na kasoro nyingi na udanganyifu. Tume ya uchaguzi CENI inakanusha hili.
Msemaji wa serikali Patrick Muyaya alisema kuwa upinzani unapaswa kusubiri hadi matokeo kamili yatakapochapishwa na kuyapinga katika mahakama ikibidi.