Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza siku ya Jumanne kwamba maandamano yaliyopangwa kufanyika Jumatano na upinzani kupinga “makosa” ambayo ulidai yaliharibu uchaguzi wa Desemba 20 na 21 yatapigwa marufuku
“Maandamano ya kesho yanalenga kudhoofisha mchakato wa uchaguzi, serikali ya Jamhuri haiwezi kukubali hili,” Waziri wa Mambo ya Ndani Peter Kazadi amewaambia waandishi wa habari. “Ninaweza kuwahakikishieni kwamba hakutakuwa na maandamano,” amesisitiza.
Katika barua iliyotangazwa kwa umma siku ya Jumamosi, wagombea urais watano wa upinzani walimfahamisha gavana wa Kinshasa kuhusu nia yao ya kuandaa maandamano siku ya Jumatano. “Tutapinga ukiukaji uliozingatiwa wakati wa shughuli za upigaji kura,” waliandika, wakielezea uchaguzi huo kama “uchaguzi bandia.”
Miongoni mwa wapinzani hao ni Martin Fayulu, mgombea ambaye alishindwa katika uchaguzi wa mwaka 2018, na Denis Mukwege, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa huduma yake kwa wanafake waathiriwa wa ubakaji katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita.
Kambi ya mgombea mwingine wa upinzani, gavana wa zamani wa mkoa wenye madini wa Katanga (kusini-mashariki) Moïse Katumbi, kwa upande wake alitoa wito wa kufutwa moja kwa moja kwa uchaguzi. Mapema Desemba 20, upinzani ulielezea uchaguzi kama “machafuko kamili”.