Waandamanaji katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamechoma moto bendera za Marekani na Ubelgiji, wakidai kuwa nchi za Magharibi zinatoa msaada kwa Rwanda, nchi jirani inayotuhumiwa kuunga mkono waasi wa M23 wanaotishia amani Mashariki mwa nchi hiyo.
Huku wakitamka nara kama vile “Ondokeni katika nchi yetu, hatutaki unafiki wenu,” baadhi ya wanaandamanaji walirusha mawe kuvunja kamera za usalama kwenye moja ya ofisi za kidiplomasia za Marekani.
Video zilizochapishwa kwenye X zinaonyesha watu wakishangilia wakati waandamanaji wakishusha bendera ya Umoja wa Ulaya kwenye lango la Hoteli ya Memling katikati mwa mji mkuu wa DRC, Kinshasa siku ya Jumatatu.
Maandamano yameshuhudiwa kwa siku kadhaa mjini Kinshasa katika ofisi za kidiplomasia za nchi za Magharibi na baadhi ya mashirika ya kimataifa kuanzia siku ya Jumamosi ambapo vijana wenye hasira wakichoma moto magari kadhaa ya baadhi ya balozi na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO).