Wagombea wa upinzani kwenye uchaguzi mkuu ambao matokeo yake yanasubiriwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wamesema wataendelea na mipango yao ya kufanya maandamano hii leo licha ya katazo la serikali.
Mmoja ya wagombea hao Martin Fayulu amesema wanasiasa wengine wote waliotishia kwa pamoja maandamanao makubwa kulaani dosari za uchaguzi huo mkuu uliofanyika Disemba 20 wataendelea na mipango hiyo kwa kuwa wanaamini uchaguzi huo ulijaa udanganyifu.
Fayulu amesema maandamano hayo yatafanyika kwa sababu upinzani hauwezi kukubali kile amekitaja kuwa “mapinduzi mengine kwa njia ya uchaguzi”.
Amezungumza saa chache baada ya Naibu Waziri Mkuu wa Kongo, Peter Kazadi, kusema maandamano yanayopangwa na upinzani hayana msingi wa kisheria na yanalenga kuvuruga kazi ya tume ya kuendelea kujumlisha matokeo.
Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi, CENI, Denis Kadima amesema tume hiyo haitosita kubatilisha baadhi ya matokeo ya uchaguzi iwapo udanganyifu utathibitishwa.
Rais Felix Tshisekedi anayewania muhula wa pili anaongoza kulingana na matokeo hayo ya awali.