Mvua kubwa imeendelea kukumba majimbo ya Ghuba, na kusababisha mafuriko makubwa na kutatiza safari za ndege katika uwanja wa ndege wa pili kwa shughuli nyingi zaidi duniani.
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai ulitahadharisha kuhusu “hali zenye changamoto nyingi” na kuwashauri baadhi ya abiria kutofika kutokana na maeneo yaliyosombwa na maji.
Kaskazini zaidi, mwanamume mmoja alikufa gari lake lilipokumbwa na mafuriko.
Huko Oman, waokoaji walipata mwili wa msichana huko Saham, na kufanya idadi ya vifo nchini kufikia 19 tangu Jumapili.
Siku ya Jumatano, takriban safari 300 za ndege kwenda na kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai – kitovu kikuu cha kuunganisha safari za ndege kwa kila bara – zilighairiwa, kulingana na data ya Flight Aware, na mamia zaidi yalichelewa.
Uwanja wa ndege, ambao mwaka jana ulihudumia zaidi ya abiria milioni 80, wa pili baada ya Atlanta nchini Marekani, ulionya kupona kutachukua “muda”.
Siku ya Jumatano ilishauri dhidi ya kutembelea Kituo cha 1 bila uthibitisho kutoka kwa mashirika ya ndege na kuepuka safari za kwenda uwanja wa ndege.
Emirates, shirika kuu la ndege la kimataifa lenye makao yake makuu mjini Dubai, lilisimamisha uingiaji kwa abiria waliokuwa wakitoka jijini humo hadi Alhamisi.
Mamlaka ilitahadharisha kuwa mvua nyingi zaidi za radi, mvua kubwa na upepo mkali zilitabiriwa, huku maeneo mengi ya mabondeni yakiwa bado chini ya maji.